Alhamisi 26 Novemba 2026 - 11:30
Uwezo wa “Theolojia ya Kijamii” Katika Njia ya Kujenga Ustaarabu Mpya wa Kiislamu/ Theolojia ya Kiislamu Ina Jukumu la Kufafanua, Kutoa Hoja, Kutetea na Kuimarisha Maarifa ya Itikadi

Hawza/ Ayatollah Arafi, akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi utambulisho wa kielimu wa ijtihadi katika elimu ya Theolojia (Ilmul-Kalam), alisema kuwa Theolojia ya Kijamii ni uwanja unaowezesha kutoa majibu yenye utaratibu na misingi ya kitaalamu kuhusu masuala na mahitaji mapya yanayoibuka katika jamii.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Alireza Arafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, Jumatano usiku, alitoa hotuba katika Mkutano wa Kitaifa wa “Falsafa ya Theolojia ya Kijamii kwa Msisitizo wa Fikra za Kikalamu za Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Iran.”

Mkutano huo uliandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Utamaduni na Fikra za Kiislamu, kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Mkutano wa Shule ya Fikra ya Imam Mujahid Shahidi pamoja na baadhi ya taasisi za kielimu na kiutamaduni nchini Iran, katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Falsafa.

Akizungumza katika mkutano huo, Ayatollah Arafi alisema: "Kuandaliwa Mkutano wa Kitaifa wa Falsafa ya Theolojia ya Kijamii kwa msisitizo wa fikra za Mheshimiwa Imam Khamenei, kunatoa fursa muhimu ya kutafakari upya nafasi tukufu ya elimu ya Theolojia, uwezo wa kistaarabu uliomo katika maarifa ya kiitikadi, pamoja na umuhimu wa kupanua wigo wa elimu hii katika kukabiliana na masuala ya jamii ya kisasa."

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Kielimu aliongeza: "Elimu ya Theolojia ni miongoni mwa elimu za msingi kabisa za Kiislamu, na ina jukumu la kufafanua, kutoa hoja, kutetea na kuimarisha maarifa ya kiitikadi. Hata hivyo, pamoja na kuhifadhi asili na utambulisho wake, haiwezi kupuuza mabadiliko katika maisha ya mwanadamu, mabadiliko ya kijamii na mahitaji ya kifikra ya jamii."

Aliendelea kusema: "Ikiwa tutazingatia kwamba maarifa ya kiitikadi yanahusiana na ukweli wa mwanadamu, ulimwengu, jamii, historia na lengo la safari ya mwanadamu, basi wigo wa athari zake hauishii katika imani za mtu binafsi pekee. Itikadi za kidini zina nafasi ya msingi katika kuunda mtazamo wa mwanadamu kuhusu jamii, uadilifu, mamlaka, uhuru, maendeleo na mahusiano ya kijamii.

"Kwa mtazamo huu, Theolojia ya Kiislamu ni msingi wa kimaarifa na kifikra kwa ajili ya Fiqhi ya Kiserikali na Kijamii pamoja na Maadili ya Kijamii, katika njia ya kujenga ustaarabu mpya wa Kiislamu."

Kutofautisha Tabaka Mbili za Maarifa

Ayatollah Arafi alisema: "Katika mwelekeo huu, ni muhimu kutofautisha tabaka mbili za maarifa:

Kwanza: Theolojia ya Kijamii (Kalam Ijtimaai). Hii ni elimu ambayo, huku ikihifadhi utambulisho wake wa Kiwahyi na mbinu yake ya kutoa hoja za kiakili na kimantiki, huchunguza kwa utaratibu uhusiano kati ya mafundisho ya kiitikadi na maisha ya kijamii.

Pili: Falsafa ya Theolojia ya Kijamii. Hii ni elimu ya daraja la pili inayochunguza dhati, misingi, mbinu, wigo, uhalali wa kimaarifa na uhusiano wa Theolojia ya Kijamii na Theolojia ya Msingi pamoja na Sayansi za Kijamii.

"Theolojia ya Kijamii bila ya kuwa na msingi wa kifalsafa na kanuni za ijtihadi, iko katika hatari ya kupanuka bila ya kuwa na mipaka na vigezo maalumu, au kuangukia katika mtego wa kupunguza masuala ya kidini na kuyatafsiri kwa mtazamo wa kisosholojia pekee, pamoja na kuiga mifumo ya theolojia ya kilimwengu ya Magharibi."

Kufungua Mielekeo Mipya kwa Kutumia Uwezo wa Ndani wa Elimu ya Theolojia

Mjumbe wa Jumuiya ya Walimu wa Chuo cha Hawza cha Qom alisema: "Lengo la Theolojia ya Kijamii ni kufungua mielekeo mipya kwa kutumia uwezo uliopo ndani ya elimu ya Theolojia. "Leo tunapaswa kuzungumzia kuundwa kwa 'familia ya elimu mbalimbali za Theolojia', ambazo kwa kutegemea ijtihadi ya kiakili na yenye utaratibu, huku zikihifadhi utambulisho wake halisi, zinatoa majibu kwa mahitaji ya zama hizi.

"Kufafanua elimu hii ndani ya mfumo wa fikra za Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi, Ayatollah Al-Udhma Imam Khamenei, kuna umuhimu mkubwa. Hii ni kwa sababu katika fikra zake, imani ya kidini si mkusanyiko wa mitazamo ya kiakili na ya mtu binafsi pekee, bali ni msingi wa kuielewa historia na chanzo cha kuwajibika kwa pamoja katika jamii."

Aliongeza: "Tauhidi na Umola wa Mwenyezi Mungu usio na mipaka katika mfumo huu wa fikra, ni msingi wa kukataa kila aina ya utawala wa mabavu, kukabiliana na taghuti, kulinda heshima na utu wa mwanadamu, pamoja na kusimamisha uadilifu."

Unabii, kwa upande wake, unahusiana na kuongoza mwanadamu na jamii, kurekebisha mahusiano ya kijamii na kuandaa mazingira ya mwanadamu kuelekea maisha yanayojengwa juu ya haki, uadilifu na kumwabudu Mwenyezi Mungu. Manabii, sambamba na kuwalingania watu katika imani, walisimama dhidi ya upotovu wa kifikra na kijamii, na walifanya juhudi za kumkomboa mwanadamu kutoka katika ujinga, dhuluma na mahusiano yasiyo ya haki.

Imama na Wilaya ni dhamana ya kuendelea kwa uongozi wa Mwenyezi Mungu, kupanga na kusimamia mambo ya kijamii, pamoja na kuelekeza mwendo wa Umma katika njia ya haki. Vilevile, kuamini Sunna za Mwenyezi Mungu kunajenga mtazamo unaotambua kwamba mabadiliko ya kijamii na kihistoria yana kanuni na malengo maalumu. Hali hii inatoa uwezekano wa kuelewa uhusiano kati ya imani, matendo, matakwa ya mwanadamu, uwajibikaji wa kijamii na hatima ya jamii.

Katika mfumo huu, mwanadamu ana uhuru wa kuchagua na wajibu ndani ya mfumo wa Sunna za Mwenyezi Mungu, na matendo yake ya kibinafsi na ya kijamii yana athari katika hatima ya ustaarabu wa jamii.

Mahitaji ya Kimkakati kwa Ajili ya Kutekeleza Mwelekeo Huu

Ayatollah Arafi alieleza kuwa kutekeleza mwelekeo huu na kuzungumzia nafasi ya Theolojia ya Kijamii kunahitaji kuzingatia mahitaji yafuatayo ya kimkakati:

1. Mabadiliko na upanuzi wa elimu ya Theolojia katika kukabiliana na masuala ya jamii.

Alisema kuwa masuala ya jamii yanapaswa kuvuka kiwango cha kuwa mada za nje ya elimu na kugeuka kuwa "mazingira yanayozalisha elimu" ndani ya Hawza. Alifafanua: "Elimu haikui katika ombwe, bali huendelea kukua kupitia kukabiliana mara kwa mara na maswali, mahitaji na uhalisia wa maisha ya mwanadamu.

2. Theolojia ya Kijamii inahitaji mbinu ya wazi na yenye mshikamano.

Ayatollah Arafi alisema kuwa ili Theolojia ya Kijamii iweze kupata nafasi inayostahili katika taaluma za kielimu na kuwa na uwezo wa kuunda na kuelekeza mjadala wa kijamii, inahitaji mbinu ya utafiti iliyo wazi na yenye mshikamano.

Alisema: "Ni lazima kubainisha tabaka za masuala ya kijamii zinazohusiana na elimu ya mwanadamu na itikadi. Katika njia hii, ni muhimu kutumia mtazamo wa uchambuzi na uhakiki matokeo yaliyopatikana katika Sayansi za Kijamii, Sayansi za Utambuzi na Saikolojia, kwa lengo la kuelewa kwa usahihi zaidi mada zinazochunguzwa.

"Hata hivyo, hukumu ya mwisho na uchambuzi wa misingi ya masuala hayo lazima daima ufanywe kwa kutumia mbinu sahihi ya kielimu ya Theolojia, huku kukiwa na mipaka iliyo wazi dhidi ya mitazamo isiyojengwa juu ya Tauhidi.

Ayatollah Arafi, katika hitimisho la hotuba yake, alisema: "Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Taasisi ya Utafiti wa Utamaduni na Fikra za Kiislamu kwa kujali kwake masuala ya kielimu na juhudi zake zenye thamani katika kubuni, kupanga na kuandaa tukio hili la kielimu. Pia ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awajaalie mafanikio zaidi waandaaji wa tukio hili, maprofesa, watafiti na washiriki wote katika harakati hii ya kielimu."

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha